Kuhusu
- Kuanzishwa kwa Baraza la Mitihani la Tanzania
- Orodha ya viongozi wa NECTA tangu kuanzishwa kwake 21-11-1973
- Kazi za Baraza la Mitihani la Tanzania
Historia ya NECTA kwa ufupi
Baada ya Tanzania Bara kujitoa katika Baraza la Mitihani la Afrika Mashariki mwaka 1971 na kabla ya Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) kuanzishwa kwa Sheria mwaka 1973, Kitengo cha Mitaala na Mitihani cha Wizara ya Elimu kilichukua jukumu la mitihani yote. Kutokana na kuanzishwa kwa NECTA, Mitihani ilikuwa jukumu lake kulingana na sheria. Mitaala iliendelea kuwa chini ya Wizara ya Elimu na Chuo Kikuu, Dar es Salaam hadi wakati ilipochukuliwa na Taasisi mpya iliyoanzishwa, inayojitegemea, Taasisi ya Ukuzaji wa Mitaala (ICD) mwaka 1975, ambayo mnamo mwaka 1993 ilibadilishwa jina na kuwa Taasisi ya Elimu Tanzania (TIE).Kati ya mwaka 1972 na 1976 wafanyakazi wa kwanza wa NECTA waliajiriwa, miongoni mwao alikuwepo ndg. P. P Gandye ambaye aliajiriwa mwaka 1972 na baadaye mwaka 1994 aliteuliwa kuwa Katibu Mtendaji. Wafanyakazi wengine waliendelea kuajiriwa na hususan wakati ofisi za NECTA zilipohama kutoka Wizara ya Elimu Makao Makuu hadi ofisi za sasa zilizo Kijitonyama karibu na Mwenge. Kwa sasa idadi ya wafanyakazi wa NECTA ni zaidi ya 250.
Kuanzishwa kwa Baraza la Mitihani la Tanzania
Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) ni Taasisi ya Serikali ambayo ilianzishwa na Sheria ya Bunge Na. 21 ya mwaka 1973. NECTA inawajibika na usimamizi wa Mitihani yote ya Taifa Tanzania.Uamuzi wa kuanzisha Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) ulikuwa ufuatiliaji wa harakati za awali za Aprili 1971, wakati Tanzania Bara ilipojitoa katika Baraza la Mitihani la Afrika Mashariki ili kusimamia mitihani yake yenyewe. Zanzibar ilijitoa katika Baraza la Mitihani la Afrika Mashariki mwaka 1970. Kabla ya kujitoa, kati ya mwaka 1968 na 1971, Tanzania ilifanya Mitihani ya Shule za Sekondari ya nje iliyoendeshwa kwa ushirikiano na East African Syndicate, ambayo kabla ya hapo iliendeshwa na Cambridge Local Examinations Syndicate pekee. Mitihani iliyoendeshwa na Cambridge Local Examinations Syndicate wakati huo ilikuwa Mitihani ya Cheti cha Elimu ya Sekondari na Mitihani ya Cheti cha Elimu ya Juu Sekondari. Mitihani ya Cheti cha Elimu ya Sekondari ilifanywa na Wanafunzi Waafrika kwa mara ya kwanza mwaka 1947 na ule wa Cheti cha Elimu ya Juu Sekondari mwaka 1960.

Comments
Post a Comment